Ujenzi wa Reli ya kisasa itakayoziunganisha Kenya, Uganda na Rwanda katika hatua nzuri
Ramani ya Reli ya kisasa itakakopitia |
Serikali ya Uganda kupitia Bunge la nchi hiyo imepitisha muswada wa
kuomba mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 2.9 kufadhili mradi wa ujenzi wa
reli kutoka eneo la Malaba mpakani na Kenya hadi mji mkuu Kampala. Rwanda
inasubiri utekelezaji wa mradi huo mpana kwa upande wa Uganda kabla ya kuanza
kuanza shughuli za ujenzi wa sehemu ya reli hiyo itakayopita katika ardhi yake.
Hatua ya Uganda inafuatia sharti ya mfadhili mkuu wa ujenzi huo, nchi ya
Uchina kuzitaka pande zote zinazohusika kwenye mradi huo wenye thamani ya
mabilioni ya Dola za Kimarekani, ikiwamo Rwanda kuridhia utekelezaji wake kwa
pamoja.
Tayari matumaini ya ujenzi wa reli ya kisasa itakayoziunganisha nchi za
jumuiya ya Afrika mashariki yalianza kupungua baada ya Uganda siku za nyuma kutangaza kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa reli ambayo ingewaunganisha na Tanzania wakiwa hawana uhakika wa kupata fedha za kugharamia ujenzi wa reli inayoelekea Kigali. Waziri wa nchi wa Rwanda anayehusika na uchukuzi, Dkt Alexis Nzahabwanimana anasema kuwa inchi yake imejipanga
kutekeleza sehemu yake ya mradi huo pindi tu serikali ya Uganda itakapokuwa
imekamilisha upande wake.
Mwanzoni
mwa mwaka huu, Uganda ilitangaza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mlaba
hadi Kampala yenye urefu wa kilometa 273 utatekelezwa na kampuni ya China
Harbour Engineering Company, ukitarajiwa kukamilika baada ya kipindi cha miezi 40.
Wahandisi wakiendelea na ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) nchini Kenya |
Hatua
ya Uganda inaongeza matumaini ya kujengwa kwa reli inayotegemewa kuanzia Mji wa
mwambao mwa Kenya wa Mombasa kupitia Uganda na hatimaye kufika mji mkuu wa
Rwanda, Kigali.
Mapema
May 31 mwaka huu, Kenya ilizindua sehemu ya kwanza ya mradi huo iliyokamilika
kwa kuziunganisha Mombasa na Nairobi, umbali wa kilometa 470. Wakati huo
ilitangaza kuendelea na awamu ya pili itakayoiunganisha miji ya Nairobi,
Naivasha na Kisumu kabla ya kuelekea mpakani mwa Uganda ambapo fedha za mradi
huo zimepatikana tayari.
Ili
kujenga sehemu ya gari ya Moshi kutoka mpakani mwa Uganda hadi Kigali, Rwanda
italazimika kugharimikia walau Dola za Kimarekani milioni 500.
Comments
Post a Comment