Urusi yajibu vikwazo vya Marekani
Urusi imejibu vikwazo vipya ilivyowekewa na Marekani kwa kutangaza kushikilia mali za ubalozi wa Marekani jijini Moscow na kuitaka nchi hiyo kupunguza idadi ya wafanyakazi kwenye ubalozi wake nchini Urusi.
Ikulu ya Urusi (Kremlin) imechukua hatua ya papo kwa papo muda mfupi baada ya baraza la Seneti nchini Marekani kupiga kura inayoidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi, Iran na Korea kaskazini huku hatua hiyo ikionekana kupingwa na Rais Donald Trump. Muswada wa Bunge la Marekani kuhusu hatua hizo mpya unasubiri kusainiwa na Rais Trump kabla ya kugeuka sheria.
Urusi imetangaza kupitia Maofisa wake wakuu kwamba Ubalozi wa Marekani jijini Moscow na ubalozi mdogo wa nchi hiyo katika miji ya St. Petersburg, Yekaterinburg na Vladivostok ni lazima wapunguze idadi ya "wanadiplomasia na watalamu" kufikia 455, huku wakitoa Septemba Mosi mwaka huu kama muda wa mwisho kufanya hivyo.
Idadi hiyo ya wafanyakazi italingana na idadi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Urusi waliopo nchini Marekani. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi pia imesema itachukua udhibiti wa ghala na jengo la starehe vinavyotumiwa na Ubalozi wa Marekani.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin (kushoto) akizungumza na mwenzake wa Marekani, Donald Trump(kulia) kwa njia ya simu (picha ya mtandaoni) |
Sheria mpya ya vikwazo nchini Marekani inalenga kuiadhibu Urusi kufuatia tuhuma za kujihusisha na uingiliaji wa Uchaguzi wa mwaka 2016 wa Rais nchini Marekani na kile kinachotajwa kuwa ni uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine na Syria, ambako Kremlin inamuunga mkono Rais Bashar Al-Assad. Sheria hiyo pi inamzuia Rais Trump kulegeza ama kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi bila ya idhini ya Congress (Bunge la Marekani).
Mwezi Desemba mwaka jana, aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama aliwafukuza wafanyakazi 35 wa Ubalozi wa Urusi nchini humo akiwatuhumu kuwa majasussi na kuchukua udhibiti wa maeneo ya Ubalozi wa nchi hiyo kwa madai ya kuingilia uchaguzi wa rais nchini Marekani. Wizara ya mambo ya nje ya urusi wakati huo ilimshauri Rais Vladimir Putin kulipa kisasi kwa kuwafukuza wanadiplomasia wa Marekani, lakini akasema angesubiri, katika kile kilichoonekana kama kuvuta subira kwamba Rais mpya angebatilisha uamuzi huo baada ya kula kiapo.
Comments
Post a Comment