Polisi 140 wa Rwanda waelekea Haiti
Polisi 140 wanaenda kuchukua mahali pa wenzao 160 wanaorudi nchini Juma hili |
Kundi la skari Polisi 140 wa Rwanda
limeondoka nchini Jumatano jioni kuelekea kwenye ujumbe wa amani wa kimataifa
nchini Haiti. Kundi hilo linalohusisha Polisi wa kike 20 linaunda awamu ya 8 ya
Polisi maalumu wa kulinda amani (FPU VIII).
Hii ni awamu ya nane ya Polisi waliopewa mafunzo maalumu (FPU) kuelekea katika ujumbe wa amani wa Umoja wa mataifa nchini Haiti. Kundi hilo linaloongozwa na Kamishna msaidizi wa Polisi Yahya Kamunuga linaunda kikosi kijulikanacho kama RWAFPU-VIII katika taifa hilo la visiwa vya Caribbean.
Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa
wa Kigali, Polisi hao 140 wameagwa na Naibu Inspekta Mkuu wa Polisi, DIGP
Juvenal Marizamunda, aliyewatakiwa heri katika kutimiza majukumu yaliyopo
mbele yao na kuwataka kuilinda hadhi ya Rwanda kimataifa.
Kwa mujibu wa msemaji wa Polisi ya
Taifa, Kamishna msaidizi wa Polisi, Theos Badege askari polisi hao watakuwa na
majukumu ambayo ni pamoja na kusaidia kulinda usalama wa wafanyakazi wa Umoja
wa mataifa nchini Haiti pamoja na vifaa vya Umoja huo, usalama wa wananchi na
mali zao pamoja na miundombinu.
Ni kundi linalochukua nafasi
itakayoachwa wazi na wenzao 160 wanaomaliza muda wao nchini Haiti na ambao
wanatarajiwa kuwasili jijini Kigali Ijumaa chini ya uongozi wa Kamishna
msaidizi wa Polisi, faustin Ntirushwa. Polisi wengine 9 wa Rwanda wapo nchini
haiti wakiwa na jukumu la kutoa mafunzo na kuwaongezea ujuzi Polisi wa Haiti.
Rwanda ni ya tatu kwa kuwa na Polisi wengi wa kulinda amani kimataifa |
Rwanda ni nchi ya tatu kimataifa kwa kuwa na idadi kubwa ya Polisi wanaohudumu katika ujumbe wa kulinda amani kimatifa. Nafasi ya kwanza inashikiliwa na Senegal ikifuatiwa na Bangladesh. Pia ni ya pili duniani kwa idadi kubwa ya Polisi wa kike wanaohudumu kwenye ujumbe kama huo maeneo tofauti ya dunia, huku ikitarajiwa kushika nafasi ya kwanza baada ya kutuma ujumbe utakaoundwa na askari Polisi wa kike pekee siku za usoni.
Comments
Post a Comment